Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango akutana na wahasibu katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akili, amesema bado kasi ya ukusanyaji mapato hauridhishi hivyo amewataka wahasibu na wakusanyaji mapato kuibua vyanzo vipya vya mapato.
Dk. Akili aliyasema hayo katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni jijini Zanzibar, alipokuwa akizungumza na Wahasibu na Wakaguzi wakuu wa Serikali katika Kikao Kazi.
Katibu Juma amesisitiza kuwa ukusanyaji mapato yasiokuwa na kodi kuwa madogo huku fursa nyingi zinaonekana za kupata mapato katika taasisi lakini suala hilo hawajaweza kulifanyia kazi ipasavyo. 
Dkt. Juma amesema Serikali inaendelea kuinua uchumi wake kupitia sekta ya utalii, ambapo eneo hilo likearhuriwa kutokana na mtikisiko wa maradhi ya corona.
Aidha, Dkt. Akili alisema wataalamu wa uchumi wamekuwa wakipata taabu wanapofanya makadirio ya mapato yasiyokuwa ya kodi, hivyo aliwataka wahasibu na wakaguzi kushirikiana na maafisa masuuli kwa kukaa pamoja na kuandaa mipango yenye tija.
“Wito wangu kwenu Kwenye hili tujue bado tuna Kazi kubwa ya kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vya vipya vya mapato”
“Bado kuna kazi nyingi za kufanya kwa wahasibu na wakaguzi na sio kuendelea kuandaa bajeti, vocha, kupitisha matumizi na mengine yanayofanana na hayo, badala yake muwe wabunifu katika kutafuta vyanzo tofautii vya mapato kwa maslahi ya Nchi yetu.
Alisema eneo la uhasibu ndio pekee lenye matumizi makubwa ya fedha, hivyo umefika wakati kwa wahasibu kuchunga nidhamu ya matumizi ya Fedha za Serikali ili kwenda sambamba na mipango bora ya maendeleo.
Nae Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani Ndg. Rashid M.Kassim alifahamisha kuwa wakaguzi wa ndani nao wahakikishe wanafuata taratibu zote ili kuhakikisha hakuna rushwa, ubadhirifu na badala yake wafuate vyema sheria ya usimamizi wa fedha za serikali.
Naibu Katibu Mkuu Ndg. Aboud Hassan Mwinyi aliwataka wafanyakazi hao kushirikiana na Afisa Masuul ili kufikia malengo ya Serikali ya yaliyokusudiwa katika kuiletea Maendeleo Nchi yetu.
Aidha, Naibu Aboud aliwataka wafanyakazi hao kubadilika na kuwa waadilifu katika kufanyakazi na kufuata utaratibu uliowekwa kisheria wa Matumizi ya Fedha za Serikali.
Baadhi ya wahasibu na wakaguzi hao, walisema katika taasisi zao wamekabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutotiliwa bajeti katika vitengo vyao na kupelekea kukwamisha utendaji kazi zao.