MAREKANI YAVUTIWA NA MAENDELEO YA ZANZIBAR.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Mhe. Jamal Kassim Ali, ameeleza kuwa Serikali ya Marekani imeahidi kuendeleza ushirikiano na Zanzibar ili kuimarisha sekta mbali mbali.

Mhe. Jamal ameeleza hayo leo mara baada ya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright, yaliyofanyika katika ofisi ya Rais Fedha na Mipango Vuga mjini Zanzibar.
Alieleza kuwa katika mazungumzo hayo, Balozi huyo kwa niaba ya Serikali ya Marekani imeahidi kuimarisha uhusiano na mashirikiano na Zanzibar na kwamba itahakikisha inasaidia kuimarisha huduma mbali mbali za kijamii.

“Tumejadiliana namna tunavyoweza kuendeleza ushirikiano lakini pia namna tutakavyoimarisha sekta ya afya, upatikanaji wa nishati ya umeme, uimarishaji wa sekta ya elimu, uhifadhi wa mazingira, utalii na uwekezaji katika ujenzi wa bandari ya kisasa Mangapwani,” alisema Mhe. Jamal.

Aidha Waziri Jamal katika mazungumzo hayo, aliiomba nchi hiyo kuwapatia fursa za kuwajengea uwezo watumishi wa umma kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na kuimarisha miundombinu ya biashara kati ya nchi mbili hizo.

Kwa upande wake Balozi Donald alieleza kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar ili kuimarisha ustawi wa jamii wa watu wake na kukuza uchumi.
Aliongeza kuwa nchi yake inajivunia mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbali mbali ikiwemo ya afya na kwamba nchi hiyo itaendelea kutoa mchango wake ili kuongeza ufanisi na mafanikio zaid.