Mhe. Jamal Kassim Ali amefanya ziara ya kutembelea Taasisi za Serikali.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Mhe. Jamal Kassim Ali amefanya ziara ya kutembelea maeneo ya matatu tofauti ya Taasisi za Serikali ili kujionea uhalisia wa kazi ya ukusanyaji wa Mapato ya Serikali. 
Mhe. Jamal alianza kutembelea eneo la Matangi ya mafuta Mtoni ili kuelewa jinsi kodi ya mafuta inavyokusanywa na Taasisi zilizopo katika eneo hilo. Nao watendaji hao walimueleza Mhe. Jamal namna wanavyotoa “Certificates of quantity”. 
Mhe. Jamal alipata fursa ya kuelezwa na kujionea jinsi mafuta yaliyoingia nchini yanavyopimwa. Kituo hicho cha Mtoni kimekusanya wafanyakazi wa Taasisi tofauti wakiwemo TRA, ZRB, ZURA na Wakala wa Vipimo.
Mhe. Jamal aliwaagiza watendaji hao kutoa ripoti ya mwezi inayohusu uingiaji wa mafuta kwa kila Taasisi iliyokuwepo katika eneo la mafuta mtoni ili kuielewesha Serikali kima cha Mafuta kilichoingia nchini na wananchi watapata uelewa

Eneo la pili alotembelea Mhe. Waziri ni eneo la Karakana, Mhe. Jamal alisisitiza mapato yakusanywe kupitia mfumo mzuri. Katika eneo hili Waziri alielezwa kuwa kwa sasa leseni za Magari zinatolewa na mamlaka ya usafiri ili kuondoa usumbufu uliokuwa ukijitokeza. 

Eneo la tatu alilotembea Mhe. Jamal ni  eneo la ZRB na kupata fursa ya kuongea na Uongozi wa ZRB. Mhe. Jamal ameiagiza Bodi ya Mapato ya Zanzibar kuhakikisha wanayafikia maeneo yote ya vianzio vya Mapato ili kuiwezesha Serikali kujipatia mapato na kufikia malengo yake.
Mhe. Jamal ameueleza Uongozi wa ZRB kuwa yeye binafsi hajaridhishwa jinsi ZRB inavyokusanya mapato kwa sasa kwani kuna maeneo mengi bado hawajayafikia katika kukusanya kodi ya Serikali. kama baadhi ya ujenzi wa Hoteli pamoja na uwekaji wa mabango wa maeneo mbalimbali.
Nae kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar Ndg. Salum Yusuf Ali ameeleza changamoto ambayo imepelekea kushuka kwa ukusanyaji wa mapato kumesababishwa na uingiaji mdogo wa wageni nchini.
Hata hivyo amesema ZRB itahakikisha inajipanga upya katika kuyafikia maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikali.