Serikali imeandaa mkutano wa majadiliano na washirika wa maendeleo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, amefunga Mkutano wa Majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliohusisha Mawaziri, Mabalozi, Sekta binafsi na Asasi za kiraiya, mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam. 

Mhe. Jamal amesema mkuno huo umetoa fursa ya Nchi kukutana na washirika wa Maendeleo na kuweza kuwasilisha mipango ya Nchi iliyopangwa ili waweze kuona namna ya kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ya Nchi iliyowekwa.

Waziri Jamal amesema kuwa mkutano huo umejumuisha sekta binafsi kwa kutambua umuhimu wake katika kuchochea ukuaji wa Uchumi na kuwa mkutano huo utaleta tija kwa ustawi na ukuaji wa uchumi wa Nchi. 

Akizungumza kwa niaba ya washirika wa Maendeleo Balozi wa Canada Nchini Mhe. Pamela O’Donnell amesema kuwa washirika wa maendeleo kwa muda mrefu wamewekeza nchini Mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuchangia maendeleo endelevu ya Nchi, na kuwa wapo tayari muda wote kuendelea kufanya hivyo katika masuala ya Elimu, Mazingira, Afya na Utawala bora kwani wanaamini kuwa fedha hizo watakazoendelea kuzitoa zitatumika kama ilivyokusudiwa. 

Balozi Pamela aliipongeza Serikali kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na kuvutia uwekezaji kwa kutunga sera, na sheria zinazovutia kwa wawekezaji ili kuja kuwekeza nchini. Vilevile Balozi aliipongeza serikali kwa kuimarisha mazingira kupitia sekta binafsi na kwa hatua hiyo itaweza kuchochea Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya watu kwa ujumla.