Serikali Mapinduzi ya Zanzibar kusaini mkataba na balozi wa Sweden

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana Saini na Serikali ya Sweden,  Jumla ya dola millioni 5.4 ambazo zitasaidia Sekta ya Elimu nchini kwa ngazi ya Maandalizi na Msingi.

Kwa upande wa Serikali ya Zanzibar Mkataba huo umesainiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Ndg. Juma Malik Akili na kwa upande wa Serikali ya Sweden umesainiwa na Balozi wa Sweden nchini Tanzania H.E. Sjoberg.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Simai amesema msaada huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kwenye Skuli ambazo zimeonekana kuwa chakavu na zenye uhaba wa vifaa pamoja na kuwasaidia Wanafunzi wenye mahitaji maalum, na kuongezea msaada huo utawasaidia Walimu wenye kiwango kidogo cha elimu ili kuwapatia taaluma kwa mujibu wa uhitaji wa masomo tofauti, elimu watakayo ipata Walimu hao itasaidia kutatua changamoto inayoikabili sekta hiyo.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, H.E. Anders Sjoberg, amesema Serikali yao itaendelea kudumisha mashirikiano na kuweza kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta hiyo. Mkataba huo utadumu kwa muda wa miaka mitano.