UFUNGUZI WA AL BARAKAH BENKI YA CRDB

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Jamal kassim Ali amesema benki ya CRDB ni benki ya mwanzo kuja na mkakati na kuonesha namna gani itashirikiana na Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili kuweza kushirikiana katika kuyafikia malengo na dira ambayo imewekwa na Serikali.
Mhe. Jamal ameipongeza benki ya CRDB kwa kushirikiana na Serikali, Pamoja na benki nyengine kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kukuza sekta muhimu za kiuchumi ikiwemo sekta ya Uchumi wa buluu ili kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika na sekta ya fedha inazidi kuimarika.
Waziri Jamal amesema wameboresha sekta ya fedha kwa lengo kuu la kuweza kuchochea ukuwaji wa Uchumi hususan sekta binafsi ambayo inawagusa wananchi wa kipato cha chini na kuwaimarisha kiuchumi ili Serikali iweze kutimiza ahadi ya Mhe. Rais ya kutoa ajira laki 3 kwa wazanzibari.
Mhe. Jamal ameyasema hayo alipokuwa akisalimiana na viongozi na wananchi waliohudhuria katika ufunguzi wa tawi jipya la CRDB benki na baadae kumkaribisha Mhe. Rais Hussein Mwinyi ili azungumze na wananchi waliohudhuria katika sherehe hizo.