Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Mhe. Dkt Saada Mkuya Salum amekabidhiwa vifaa vya ICT kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Mhe. Dkt Saada Mkuya Salum Leo, Mei 14, 2022 amekabidhiwa vifaa vya ICT kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na Balozi mdogo Mkaazi wa Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.

Mhe. Saada Mkuya ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China Kwa juhudi zao za mara kwa mara katika kuisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Aidha, Dkt. Mkuya ameeleza kuwa vifaa hivyo ni pamoja na Kompyuta 25, Laptop 8 na Vishikwanbi (IPAD) 50. Dkt. Saada amesema vifaa hivyo vitatumika katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi Agosti 23, 2022 na gharama ya vifaa hivyo ni jumla ya Tsh.107 Milioni. Nae Kaimu Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Mashavu Khamis Omar ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China Kwa msaada huo na kuahidi kuwa vifaa hivyo vitumika katika kazi ya Sensa ya Watu na Makaazi Agosti 23, 2022.

Mhe. Balozi mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China Zanzibar, Mhe. Zhang amesema China itaendelea kuisaidia Tanzania na Zanzibar katika Miradi ya Kiuchumi na Kijamii hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi 2022.