Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Saada Mkuya Salum afanya ziara ya Taasisi ya Mtakwimu Mkuu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Taasisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ni Taasisi muhimu sana kwa ajili ya Mipango na maendeleo ya Nchi. Waziri amesema Serikali inapata kujipima kimaendeleo kwa kutumia data ambazo ni sahihi ambazo zinapatikanwa katika taasisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali. Aidha, Waziri Dkt.

Saada ameiagiza Taasisi hiyo kuhakikisha wanatoa data sahihi ambazo zinapelekea kutumika katika mipango ya Nchi na ifikapo mwaka 2050 Zanzibar kuingia katika Uchumi wa kati na suala hilo linaenda sambamba na kujua kwa kuimarika kwa pato la mtu mmoja mmoja ili kuelewa hali halisi ya Uchumi wa Zanzibar. Dkt. Saada amesisitiza kwa Taasisi hiyo kuwa lazima tuwe na takwimu zinazotokana na Taasisi hii na kuelekeza kuwapatia mafunzo watakwimu waliopo sehemu nyengine ili kuandaa takwimu sahihi na kujua vyanzo vya takwimu zinazopatikana na kutumika katika Ofisi mbali mbali. Mheshimiwa amesema suala hilo litapelekea kuongezeka kwa ajira nchini.

Nae Kaimu Mtakwimu Mkuu wa Serikali Bi Mashavu ameelezea mikakati ya Ofisi hiyo ikiwemo kukusanya, kuchambua na kuchapisha takwimu za Serikali ili kuimarisha malengo ya Serikali. Ofisi ya Mtakwimu imeyachukuwa yale yote waliyoelekezwa na Mhe. Waziri. Mheshimiwa Waziri ametembelea Taasisi hiyo kwa lengo la kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Kushika wadhifa huo.