BOT Yasihiwa Kuimarisha Uchumi wa Kidijitali
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema nchi inategemea kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato ya ndani hususan yatokanayo na kodi, ambayo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi.
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akil, aliyasema hayo wakati akizungumza na watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania Ofisi ya Zanzibar mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea makao makuu ndogo Kinazini.
Alisema mapato hayo ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa shughuli za serikali na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Dk. Juma alisema tafiti zilizofanywa na wataalamu kutoka Tume ya Mipango zimebaini kuwa Zanzibar inapoteza zaidi ya asilimia 83 ya mapato ambayo ingeweza kuyakusanya endapo kungekuwa na mifumo imara na ya kisasa ya ukusanyaji wa mapato.
Alibainisha kuwa upungufu huo unatokana na kutokuwepo kwa mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, hali inayosababisha serikali kukusanya takribani asilimia 17 tu ya uwezo wake halisi.
Aidha alisema endapo mifumo ya kidijitali itatumika kikamilifu, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia asilimia 100 ya makusanyo, hivyo kuziba pengo la upotevu wa mapato unaofikia asilimia 83 ambayo kwa sasa nchi inashindwa kuyakusanya na nchi inapoteza mapato yake.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa uchumi wa kidijitali, alisema ni lazima sekta ya fedha ihakikishe kila senti inayopaswa kukusanywa inakusanywa ipasavyo na kuelekezwa katika malengo yaliyokusudiwa, yakiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida ya serikali ili kuleta tija kwa wananchi wanaoitegemea serikali yao.
Alibainisha kuwa matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali yataiwezesha nchi kujenga miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea kwa kiasi kikubwa mikopo.
“Nchi inaweza kujenga miradi yake mikubwa bila ya kukopa fedha nyingi hivyo BOT endeleeni kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna gani ya kutumia mifumo ya kisasa ya kifedha ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali,” alisema
Dk. Juma alisisitiza kuwa ni lazima nchi iendelee kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo hususan ile ya kimkakati, akibainisha kuwa mapato ya ndani yakikusanywa ipasavyo yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi kwa ujumla.
Dk.Juma aliitaka BOT kuendelea kushirikiana kwa karibu na sekta mbalimbali za uchumi pamoja na taasisi za utafiti ili kufanya tafiti zenye tija zitakazosaidia kubaini fursa, changamoto na mikakati bora ya kukuza uchumi wa nchi.
Alisema tafiti hizo ni nguzo muhimu katika kutoa mwelekeo sahihi wa sera za fedha na maendeleo kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa tafiti zinazozingatia hali halisi ya uchumi zitasaidia pia kuimarisha uthabiti wa kifedha na kudhibiti changamoto za mabadiliko ya soko la ndani na kimataifa.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Benki Kuu katika kuimarisha tafiti na ukusanyaji wa takwimu sahihi ili kuweka mazingira wezeshi ya maendeleo ya kiuchumi kwani kufanya hivyo nchi itaendelea kujenga uchumi imara.
Alisema serikali imeunda Wizara ya Mawasiliano Teknologia na Ubunifu ambayo imepewa jukumu mama la kuhakikisha uchumi wa kidijitali unatumika ipasavyo.
Aliipongeza BOT kwa kazi nzuri wanayoifanya kwani mchango wao ni mkubwa kwa serikali hivyo uzalendo , uaminifu na uadilifu ndio msingi imara wa kuendeleza kukuza uchumi wa nchi.
Akitoa taarifa ya utendaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mkurugenzi wa benki hiyo Ofisi ya Zanzibar Ibrahim Joseph Malogoi alisema benki kuu kimsingi jukumu lake ni kutekeleza kazi za msingi za nenki kuu ya Tanzania.
Hata hivyo alisema Benki Kuu inaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi kama mhifadhi na mlipaji mkuu wa SMZ na taasisi nyengine za SMT zinazofanya shughuli zake Zanzibar.
“Katika kutimiza wajibu huu benki kuu imeendelea kuhakikisha usimamizi thabiti wa akaunti za serikali, uratibu wa miamala yote ya kifedha na utoaji wa huduma za kibenki kwa wakati na ufanisi,” alisema
Hata hivyo, alisema hadi Disemba 2025 idadi ya benki za biasjara zinazofanya kazi Zanzibar ni 15 zenye mtandao wa matawi 43.
Mkurugenzi Ibrahim alibainisha kuwa makao makuu ndogo ya BOT inaendelea kuhifadhi fedha za SMZ zinazotokana na kodi na zisizotokana na kodi na kuipatia serikali hali halisi ya kifedha kila siku ili iweze kufahya maamuzi sahihi na kuhifadhi, kutoa na kusambaza fedha kwa benki za biashara zilizopo Unguja na kusimamia shughuli za uendeshaji wa kituo cha usambazaji wa noti na sarafu kilichopo Pemba ili kuhakikisha kuwa kuna fedha za kutosha katika mzunguko kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Majukumu mengine alisema ni kuhaulisha fedha na kutoa vitabu vya hundi kwa wizara na idaea mbalimbali za SMZ , kuchambua fedha ili kuzirudisja kwenye mzunguko wa fedha zilizo safi na kuziondoa kwenye mzunguko zile zilizochakaa na kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuzitambua alama za usalama za noti zao, utunzaji bora wa noti na sarafu na kuhimiza matumizi ya mifumo mengine ya malipo.
Sambamba na hayo benki pia inafatilia mwenendo wa uchumi wa Zanzibar kwa kufanya uchambuzi ikiwemo uzalishaji, mwenendo wa mapato na matumizi ya serikali, maendeleo ya sekta ya nje, mwenendo wa deni la serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na maendeleo ya sekta ya fedha.
Alifahamisha kuwa benki pia hufanya tafiti mbalimbali ikiwemo utafiti wa hali ya uwekezaji Zanzibar, itafiti wa sekta ya utalii, utafiti wa upatikanaji wa chakula na tafiti nyengine.
Alisema katika mwaka huu wa fedha shughuli za miradi mbslimbsli ilipangwa kutekelezwa ambapo hadi kufikia Disemba mwaka 2025 benki kuu Zanzibar imeendelea kutimiza jukumu lakw la kusambaza fedha (noti na sarafu) ili kutosheleza mahitaji ya uchumi bila kusababisha mabadiliko ya kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma.
Alisema katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2025 benki kuu ilisambaza jumla ya shilingi bilioni 465.6 kati ya fedha hizo bilioni 394.3 zilisambazwa kupitia ofisi ya Unguja na shilingi bilioni 71.3 kupitia kituo cha Pemba.
Alisema pamoja na mafanikio hayo zipo baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ambazo ni pamoja wananchi kutokuwa na uelewa mzuri kuhusu majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania, kutokuwa na uelewa wa fersa za uwekezaji katika masomo ya kifedha, kutokuwa na uelewa wa kutosha wa kuzitambua noti halali na namna bora ya utunzaji wa fedha.
Alisema ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya BOT una mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya fedha na kuleta utulivu wa kiuchumi.










