Serikali Yaitaka ZHSF Kuimarisha Uendelevu wa Kifedha
WIZARA ya Fedha na Mipango Zanzibar, imeutaka Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) kuhakikisha unaendelea kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za afya huku ukidumisha uendelevu wa kifedha wa mfuko huo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Wizara hiyo Dk.Juma Malik Akil wakati alipokutana na Bodi ya Wakurugenzi pamoja na watendaji wa mfuko huo, katika ziara yake ya kujitambulisha katika ofisi za mfuko huo Michenzani Moll.
Alisema ni muhimu kwa mfuko kujipanga kikamilifu ili kuendelea kuwa endelevu (sustainable) kwani mifuko inayotoa huduma za kijamii mara nyingi hukumbwa na changamoto ya kupoteza uendelevu kutokana na ugumu wa kupima faida za huduma hizo.
Aidha alisema uendelevu wa mfuko ni nguzo muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kutolewa kwa wananchi bila kuyumba.
“Ni muhimu kujipanga vizuri ili mfuko uwe endelevu, kwani hilo litahakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa uhakika na kwa muda mrefu,” alisema.
Dk.Juma alibainisha kuwa bado hana uhakika kama mfuko unaweza kuingia kwenye uwekezaji mkubwa kutokana na hatari (risk factors) zilizopo, hivyo alisisitiza fedha zinazopatikana zielekezwe kwenye miradi yenye tija na usalama zaidi.
Hata hivyo, alisema serikali imefanya maboresho ya mfumo wa ukusanyaji wa fedha za wanachama, pamoja na kuandaa utaratibu maalum wa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuongeza mapato ya mfuko, ambapo kwa awamu ya mwanzo umeanza kwa kuhusisha bima ya wasafiri.
Aliahidi kwamba serikali itaendelea kutafuta watu ambao wataweza kusaidia mfuko ili kuongeza uwezo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Hamad Omar, aliutaka mfuko huo kuhakikisha unasimamia kikamilifu sheria na kanuni zake, hususan kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu katika matumizi ya huduma za mfuko.
Alisema yapo malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu utoaji wa huduma pamoja na kutokuelewa mipaka ya huduma zinazotolewa na mfuko huo hivyo aliusisitiza mfuko kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma ili wananchi wawe na uelewa sahihi wa mfuko na haki zao.
Aliwataka watendaji wa mfuko kutanguliza misingi ya uadilifu, uzalendo na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili lengo la kuanzishwa mfuko huo liweze kufikiwa
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar, Mbarouk Omar Mohammed, aliipongeza serikali kwa kuipa kipaumbele sekta ya afya kwani kuanzishwa kwa mfuko huo kumesaidia kuwapa wananchi uwezo wa kupata huduma za matibabu kwa urahisi zaidi.
Alifahamisha kuwa hadi sasa mfuko umefanikiwa kusajili takribani asilimia 50 ya walengwa, huku asilimia nyingine ikiwa bado haijafikiwa, hususan kundi la wastaafu ambao wengi wao bado wako nje ya mfumo wa kupata mafao ya afya.
Alisema bodi inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kundi hilo halibaki nyuma na kuiomba serikali kupitia wizara husika kulifanyia kazi suala hilo ili wastaafu nao waweze kunufaika na huduma za afya kupitia mfuko huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa ZHSF, Khalifa Muumin Hilal, alisema mfuko huo unaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali wakati wa kuanzishwa kwake.
Alieleza kuwa ZHSF imeanzishwa kwa mujibu wa sheria Namba 1 ya mwaka 2023, ikiwa na lengo la kuwa mfuko imara wa kuwawezesha wananchi wote kupata huduma za afya kwa uhakika.
Aliongeza kuwa mpango wa mfuko ni kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kufungua ofisi 11 katika maeneo mbalimbali ikiwemo Tumbatu, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na ukusanyaji wa michango ya wanachama.
Alifahamisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili na nusu, mfuko ulilenga kusajili zaidi ya wanachama milioni moja (1,000,000), ambapo hadi Desemba mwaka jana, jumla ya wanachama 999,111 walikuwa tayari wameshasajiliwa.
Kwa upande wa michango, alisema mfuko ulilenga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.4, lakini hadi sasa umefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 111.
Hata hivyo, alibainisha kuwa mfuko unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo maslahi ya watendaji, matumizi mabaya ya kadi za wanachama, michango ya wastaafu, upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, pamoja na changamoto ya ofisi kwani kwa sasa mfuko unatumia jengo la kukodi.
Alisema licha ya changamoto hizo, mfuko unaendelea kuimarisha mifumo yake ya kazi, kusajili vituo vya kutolea huduma na kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya.
Aliongeza kuwa hadi sasa jumla ya vituo vya afya 135 vimeshasajiliwa kutoa huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar na hata kwa Tanzania bara.








