Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kuimarisha sekta ya ardhi kwa kujenga masjala za kisasa zitakazowezesha uhifadhi kumbukumbu na taarifa za ardhi kwa mfumo wa kidijitali, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma na kupunguza migogoro ya ardhi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akili, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Hamad Bakar, wakati wa uzinduzi wa Masjala ya Ardhi Makunduchi, alisema Serikali imeamua kwa makusudi kuwekeza katika ujenzi wa masjala hizo ili kuimarisha usimamizi wa taarifa za ardhi nchini.
Alisema mfumo huo wa kidijitali utawapa wananchi uhakika wa umiliki wa ardhi zao na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, aliitaka Kamisheni ya Ardhi kuhakikisha inakitumia kituo hicho kama kilivyokusudiwa ili kuimarisha mipango bora, imara na endelevu ya usimamizi wa ardhi.
Aliongeza kuwa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango inaendelea na ujenzi wa masjala nyingine katika Wilaya ya Chake Chake, Pemba, katika Kijiji cha Pujini.
Amesema uhifadhi wa taarifa na nyaraka za ardhi ni muhimu katika kuzuia upotevu wa kumbukumbu na kupunguza migogoro ya ardhi isiyo ya lazima.
Amefahamisha kuwa kupitia mfumo huo utasaidia kuondoa dhuluma zinazoweza kujitokeza katika umiliki wa viwanja, kuiwezesha Serikali kuwa na kumbukumbu sahihi za ardhi, pamoja na kurahisisha shughuli za uhamishaji wa umiliki na utoaji wa hati kwa wananchi na wawekezaji.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Dk. Afua Mohamed, amesema, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi inaendelea kutekeleza sera na mipango mbalimbali inayolenga kuimarisha usimamizi wa ardhi na kuimarisha utoaji wa huduma.
Amesema Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi imekuwa ikiandaa mipango mbalimbali ya kuimarisha usimamizi wa ardhi nchini.
Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana, sekta ya ardhi bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upotevu wa nyaraka muhimu za ardhi.
Amesema Dhamira ya Serikali ya kujenga kituo hiki ni kuimarisha mifumo ya utunzaji wa taarifa na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa ardhi
Ameleza kuwa ogezeko la mahitaji ya ardhi mwaka hadi mwaka linaifanya miundombinu hiyo kuwa muhimu, kwani kutokuwepo kwake kungeendelea kusababisha migogoro mingi ya ardhi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhaza Gharib Juma, alisema masjala hiyo itakuwa hazina muhimu ya taarifa za ardhi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto za uhifadhi.
Amesema vituo hivyo vina umuhimu mkubwa kwa kuwa vitatunza taarifa nyeti za taifa, hivyo akaomba viwekwe uzio kwa ajili ya kuimarisha usalama wake.
Aidha, alisisitiza kuwa kutotambuliwa kwa ardhi kwa usahihi ndiko kunakochangia kuongezeka kwa migogoro mbalimbali, hususan ya mipaka.
Ujenzi wa Masjala ya Ardhi Makunduchi umegharimu jumla ya shilingi milioni 560 hadi kukamilika kwake.