

Wizara ya Fedha na Mipango imefanikiwa kusaini mkataba wa ujenzi kupitia Mradi wa BIG-Z unayohusu kuimarisha maeneo ya utalii katika vijiji vya Chwaka na Makunduchi. Mradi wa kuimarisha maeneo ya Utalii unaratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ambao ndio wadau wakuu wanaosimamia mradi huu.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika tarehe 11 Agosti, 2026, ambapo mkataba huo umesainiwa rasmi na Kaimu Katibu Mkuu Ndugu. Aboud H. Mwinyi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ndg. Suhaila Salum Mbarak ambae ni Katibu kutoka kampuni ya SECCO (SMC-Private) Limited.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Ndugu Aboud Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa kazi za ujenzi, usimamizi mzuri wa muda pamoja na uratibu madhubuti wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, alimtaka mkandarasi kufanya kazi kwa uweledi ili kukamilisha mradi huu kwa wakati uliopangwa kwa mujibu wa Mkataba na kwa gharama iliyopangwa. Pia mkandarasi huyo alitakiwa kuhakikisha kuwa na mpango kazi ulioandaliwa vizuri ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo hauleti usumbufu kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotekelezwa miradi hiyo.
Kwa upande wa mkandarasi ameahidi kuyafanyia kazi yale yote ambayo yameanishwa katika mkataba pamoja na kuyapokea yaliyoelezwa na Mhe. Aboud. Pia ametoa shukrani kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuiamini kampuni yao kwa kuwapa kazi kubwa kama hii hasa kwa kuwa Utalii ni suala muhimu sana katika Visiwa vya Zanzibar.
Mradi wa Kuimarisha Maeneo ya Utalii Katika Vijiji vya Chwaka na Makunduchi unadhamiria kuboresha nyuumba za kihistoria za Sultan Rest House na British Rest House, maeneo ya bustani na soko la Samaki katika Kijiji cha Chwaka pamoja na kuimarisha maeneo ya wazi likiwemo eneo la Kiutamaduni la Sherehe za Mwaka Kongwa lililopo katika Kijiji cha Makunduchi.