Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil, amebainisha vipaumbele tisa vya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, vikiwemo kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kusimamia utekelezaji wa bajeti inayozingatia usawa wa kijinsia pamoja na kupitia sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma za Serikali.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika kikao cha 30 cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Chukwani, Dkt. Juma amesema wizara hiyo itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuweka mazingira bora yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Bakari Hamad Bakar, amesema kamati hiyo inashauri wizara kuhakikisha kunakuwepo na matumizi yenye tija ya fedha za umma ili mipango iliyopangwa iweze kutekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Wakati huo huo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia hotuba hiyo wamesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Akijibu hoja za wajumbe, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil, amesema Serikali itaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo yote yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Zanzibar.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliipitisha bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ya zaidi ya shilingi trilioni nane kwa ajili ya kutekelezav majukumu na vipaumbele vilivyoainishwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.