Wizara ya Fedha na Mipango imekabidhi kwa Afisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Malumu za SMZ gari za usafi 26 ikiwemo Tipper 15 na Compactor 11 Kwa ajili ya ukusanyaji wa taka ngumu katika Manispaa za Unguja na Pemba.
Hafla ya Makabidhiano hayo ilifanyika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango tarehe 8 September 2026 katika Ukumbi wa Tume ya Mipango na kushuhudiwa na watendaji wa Wizara zote mbili.
Ununuzi wa magari haya ulifanyika kupitia taratibu za ununuzi za Mradi wa BIG-Z kwa kuzingatia masharti na taratibu husika za manunuzi za Benki ya Dunia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Magari haya ni mapya na yanatumia teknolojia ya kisasa ambayo yatasaidia katika usimamizi na udhibiti wa matumizi yake. Kwa mfano: Magari ya Compactor yatafungwa GPS na kamera maalumu kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa matumizi yake na kuimarisha ufanisi wa madereva watakaotumia magari hayo.
Akizungumza katika Makabidhiano ya gari hizo, mgeni rasmi Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akil amesema hana shaka kuwa magari hayo yatatumika kama yalivyokusudiwa kutokana na imani kubwa ya Utendaji na Usimamizi kwa Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ.
Kiujumla gari hizo zimewekewa lengo la ukusanyaji na usafirishaji wa taka, kuboresha usafi wa mazingira katika maeneo yanayohudumiwa na Manispaa, usafirishaji wa vifaa na taka kwenda maeneo maalumu ya utupaji, kusaidia shughuli za usimamizi wa jaa kuu la Kibele na maeneo mengine yanayohusika, kupunguza changamoto ya uhaba wa vitendea kazi katika Serikali za Mitaa na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Dkt. Juma Malik Akil amesema Serikali inalengo la kuweka miji katika hali ya usafi na haiba ya kuvuti Kwa kununua gari maalum za ukusanyaji wa taka ngumu kupitia mradi huu.
Kaimu katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Aboud Hassan Mwinyi amesema jumla ya Bilioni 7 TSh, ndizo zimetumika katika ununuzi wa gari hizo ambazo zimetengenezwa kutoka kiwandani kama toleo la mwaka 2026 chini ya usambazaji wa kampuni za GF Trucks and Equipment Limited ya Dar es Salaam na Kampuni ya GANSU CONSTRUCTION INVESTMENT HEAVY INDUSTRY TECHNOLOGY CO.LTD ya CHINA
Nae Mhe. Idrisa Kitwana Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ
ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango Kwa kukabidhi gari hizo kwani kumekuwa na mahitaji makubwa ya magari ya ukusanyaji taka katika manispaa zote za Unguja na Pemba.
Wakati huohuo Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Tamisemi ilisaini hati ya makubaliano ya gari hizo.