Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itaendelea kuwasimamia wazee ili waishi kwenye mazingira mazuri na kupatiwa mahitaji yote yanayostahiki.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akil amesema hayo wakati akifungua kongamano la wazee ikiwa ni kuelekea siku ya wazee duniani.
Amesema Serikali imekuwa ikifatilia kwa karibu changamoto zinazowakabili wazee ili kuhakikisha wazee hao wanaishi katika mazingira bora na salama, wazee wamekuwa na mahitaji mengi yanayowakabili hivyo Serikali itaangalia kwa karibu ili kuweza kuyatatua.
Aidha amefahamisha kuwa Serikali itaangalia namna ya kuzigatia umri wa uzee kutoka miaka 70 ya sasa na kuwa miaka 60.
Hata hivyo amewataka wazee hao kuwa na tabia ya kuangalia afya zao kila baada ya muda ili kuweza kubaini maradhi yanayowasumbua.
Nae Katibu wa Jumuiya ya Wazee Wastaafu Bi Salama ameishukuru Serikali kwa kuwaongezea wazee pencheni pamoja na kuanzisha Mabaraza ya Wazee.