WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil, amezitaka sekta binafsi nchini kushirikiana kwa karibu na Serikali katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa Miaka Mitano wa Awamu ya Pili (ZADEP II), ili kufanikisha malengo ya maendeleo na kukuza uchumi jumuishi.
Dk. Akil alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa kujadili utekelezaji wa ZADEP II uliowakutanisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo, huko Golden Tulip Uwanja ndege Zanzibar.
Alisema ushiriki wa sekta binafsi unapaswa kwenda zaidi ya kuhudhuria mikutano pekee bali ni kuwa sehemu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo, ambapo Serikali pekee haiwezi kufikia malengo ya maendeleo bila ushiriki madhubuti wa sekta hizo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Mipango ya Kitaifa na Maendeleo ya Kisekta kutoka Tume ya Mipango Zanzibar Mohemed Masoud Salim alisema Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 inalenga kuifikisha Zanzibar katika hadhi ya uchumi wa kipato cha kati cha juu ifikapo mwaka 2050 kupitia maendeleo endelevu na jumuishi.
Alieleza kuwa Dira ya Zanzibar 2050 imejengwa katika nguzo nne kuu ambazo ni mageuzi ya kiuchumi, maendeleo ya rasilimali watu na huduma za kijamii, miundombinu na uunganishaji pamoja na utawala na ustahimilivu.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Josephine Rogate Kimario alisema mkutano huo umelenga kuwakutanisha Serikali na sekta binafsi ili kujadili namna ya kufadhili na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa Miaka Mitano wa Awamu ya Pili .