Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

wizara ya Fedha na Mipango

Habari & Matukio

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Zanzibar Sukuk1 Limited, Juma Amour Mohamed, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, kwa maono na juhudi zake za kuanzisha mfumo wa hati fungani za Kiislamu (Sukuk), akisema hatua hiyo ni ya kihistoria katika kuimarisha sekta ya fedha visiwani humo.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya hatua hiyo, Juma alisema Zanzibar inalenga kuwa kitovu cha huduma za fedha za Kiislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alieleza kuwa kuanzishwa kwa hati fungani zinazoendeshwa kwa misingi ya Sharia kumejibu kilio cha muda mrefu cha taasisi za fedha za Kiislamu zilizokuwa zikikosa fursa salama za uwekezaji.

Alisema kabla ya kuanzishwa kwa Sukuk, benki na taasisi nyingine za kifedha zilizokuwa zikitoa huduma za Kiislamu zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya ukwasi mkubwa (liquidity) bila kuwa na maeneo yanayokubalika kisheria kwa uwekezaji.

Hali hiyo ilisababisha kupungua kwa ufanisi wa utendaji katika soko la fedha.

“Benki za Kiislamu zilikuwa na fedha nyingi lakini hazikuwa na miradi au dhamana zinazokidhi matakwa ya Sharia kwa ajili ya kuwekeza. Hii iliathiri utendaji wao na hata kuwanyima watu binafsi fursa za uwekezaji halali,” alisema.

Aliongeza kuwa kuanza kwa Sukuk kumesaidia kukamilisha mnyororo wa mfumo wa fedha za Kiislamu, kwa kuwezesha taasisi na watu binafsi kuwekeza, kupata mapato halali na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Juma aliishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mpango huo, akisema umefanikiwa kama ulivyopangwa na kuleta matokeo chanya katika soko la fedha.

Alibainisha kuwa mfumo wa Sukuk unatumiwa na mataifa mbalimbali duniani kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo, na si nchi za Kiislamu pekee.

Alitolea mfano nchi kama United Kingdom na Belgium, ambazo pia zimetumia mfumo huo kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Sukuk1 Limited, Masoud Rashid Mohamed, alisema taasisi hiyo imeanzishwa mahsusi kusimamia miamala ya Sukuk kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, kuanzia hatua ya utoaji (issuance) hadi usimamizi wake.

Alisema tayari taasisi hiyo imeanza kutoa gawio la awali kwa wawekezaji na kufanya tathmini ya utekelezaji wake ili kubaini changamoto na kuzitatua mapema.

Aidha, katika bajeti ya mwaka huu, wamepanga kuanzisha mfumo wa kidijitali utakaorahisisha uendeshaji wa miamala hiyo, ambapo unatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi katika robo inayofuata ya mwaka wa fedha.

Masoud alieleza kuwa taasisi mbalimbali za Serikali zimeonesha nia ya kutumia mfumo wa Sukuk kufadhili miradi yao ya maendeleo, ikiwemo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), kwa lengo la kutatua changamoto za upatikanaji wa umeme visiwani humo.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Juma Ali Malik, ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kuhakikisha mfumo wa Sukuk unakuwa endelevu na unachangia kikamilifu maendeleo ya Zanzibar.

Waziri Malik alisema kuanzishwa kwa Zanzibar Sukuk1 Limited ni hatua ya kimkakati inayolenga kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya Serikali bila kuongeza mzigo wa mikopo yenye riba.

Alibainisha kuwa kupitia Sukuk, Serikali itaweza kufadhili miradi ya kimkakati ya miundombinu, nishati na huduma za jamii kwa njia inayokubalika kisheria na kidini.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kisheria na kiudhibiti ili kuimarisha zaidi soko la fedha za Kiislamu, akisisitiza kuwa dhamira ya Zanzibar ni kujijenga kama kitovu cha huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya Sharia katika ukanda huu.

Scroll to Top