WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk.Juma Malik Akil, ameiomba kamati ya Bajeti na Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hisabu za Serikali (PAC) kuwa karibu na wizara ya fedha katika kuvilinda na kuvitetea vipaumbele ambavyo vitapendekezwa na serikali na baraza liweze kuvibariki.
Dk.Juma aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa kamati hizo katika ukumbi wa Dk.Shein ZURA Maisara yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa serikali.
Alisema serikali imepita katika mageuzi makubwa katika miaka mitano na haijasita kwani inahamu kufanya mageuzi makubwa zaidi hasa kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Aidha alisema katika kufanya hivyo wanaweza kuwa na mabadiliko katika utekengezaji wa bajeti zake kwani mwaka jana waliweza kufanya bajeti takriban trillion 6.9 ikiwa ni tofauti na bajeti za miaka mitano iliyopita.
Alisema ndani ya bajeti hiyo pia waliweka vipaumbele hasa ambapo sehemu kubwa ya vipaumbele hivyo ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo mwaka jana wametekeleza kwa asilimia 63 ya bajeti nzima ukilinganisha na asilimia 37 ya kazi za kawaida za kila siku.
” Mnaweza kuona jinsi miradi ya maendeleo inavyoonekana wazi kwa kutumia mfumo huu wa kutoa kipaumbele katika bajeti zetu za serikali za miradi ya maendeleo,” alisema
Alisema mwaka huu pia serikali ina vipaumbele vyake na tayari wameshaanza michakato wa kuvitengeneza kwa kipindi cha bajeti ya 2026/2027 na miaka mitano ijayo ambayo sehemu kubwa ni kutekeleza ilani ya CCM ya 2015/2030.
Alisema pia serikali ina mkakati maalum katika kukusanya mapato kwani ndio roho ya serikali na bajeti ni mapato na matumizi na mara nyingi wamekuwa wakilenga zaidi kwenye matumizi.
Waziri Malik alibainisha kuwa wanatamani kupitia kamati kuibua mbinu mpya za mapato kwani serikali imekuwa ikipoteza mapato mengi kutokana na njia zilizoeleka.
“Mtusaidie tufanye nini ili kuepuka upotevu huu wa mapato na kushindwa kukusanya kwa sababu mbalimbali ambazo nyengine inawezekana kama tutaweza kuzisimamia vizuri zaidi,” alisema.
Alisema serikali hivi sasa inafanya mageuzi kutoka katika mfumo wa fedha taslim (Cash Base) na kutumia mfumo wa kielektroniki lengo ni kuimarisha utendaji baada ya kuona kasoro ambazo zilijitokeza katika mfumo uliopita hasa katika utambuzi wa mali za serikali na ahadi za kifedha zinazowekwa hazipati nafasi kuonekana wazi wazi wakati walipokuwa wakitumia.
Alifahamisha kuwa lengo la kuhama huko na kwenda kwenye ‘Acruare Base Aproch’ ni kuhakikisha hayo yote yanapatikana na kwenda sambamba na taratibu za kidunia.
Alisema ni matumaini yake kwamba wakipatiwa mafunzo wataweza kuyachukua na kuweza kuwasimamia vizuri zaidi katika utekelezaji wake.
“Utekelezaji wa shughuli zetu za kila siku wizara inategemea sana msaada wa kamati zetu hizi mbili kwani zinagusa mnasaba wa utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema.
Hata hivyo, alisema siku za nyuma ipo mifano ambayo wanatafutiana katika mambo fulani kutokana na kukosa uelewa lakini anaamini watazungumza lugha moja hasa wakati wa kutengeneza bajeti, kutekeleza bajeti na hata kutathimini bajeti watakuwa pamoja na wizara kusaidia kujenga hoja ili watakapowasilisha bajeti zao wawe na wenzao ambao wanawasaidia ndani ya baraza.
Dk. Juma akiizungumzia kamati ya PAC alisema wizara inapata changamoto wakati wanapopata ripoti za CAG hivyo ni matumiani yake kamati hiyo itaweza kuwasaidia mapema ili kusiwe na kasoro ambazo zinajitokeza.
Alisema kamati hizo zina umuhimu mkubwa kwani zingusa moja kwa moja utendaji wa ofisi yao hivyo alizipongeza kamati hizo kwa kukubali kupokea mafunzo na kushiriki kikamilifu.
Naye Mhasibu Mkuu wa Serikali, Hamad Saleh Hamad, alisema mafunzo hayo yamelenga kutoa uelewa kwa kamati hizo juu ya sheria ya fedha ya usimamizi wa fedha za umma ya mwaka 2016.
Alisema sheria hiyo ina mambo mengi lakini wameona wajikite katika maeneo matatu ambayo ni muhimu hasa usimamizi wa fedha za umma,usimamizi wa matumizi na matumizi ya viwango kwa taasisi za umma.
Haya ni mambo ya msingi na yanahitaji upekee kwa wajumbe wa kamati hizi kuweza kuelewa lakini pia usimamizi wa fedha kwani ndio msingi mkuu wa matumizi ya serikali lakini pia kufuata viwango vya kimataifa kwani hilo ni takwa la kisheria.
Katika mafunzo hayo mada mbalimbali ikiwemo usimamizi wa matumizi katika sekta za umma na usimamizi wa fedha za umma kutoka kwenye mfumo wa fedha taslim na kutumia mfumo wa kielektoniki.







