Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

wizara ya Fedha na Mipango

Habari & Matukio

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil amesema mashirika ya umma yanawajibu wa kuisaidia na kuichangia Serikali kupitia gawio na mapato mengine,

Dk. Akil aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea Mashirika yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa lengo la kuangalia mwenendo wa Mashirika hayo na kupokea maoni Kwa wakuu mashirika

Alisema mashirika mengi hayafanyi vizuri na yameshindwa kujiendesha, hali inayopelekea  kuwa mzigo kwa Serikali,

Aliwataka watendaji wa taasisi hizo kutimiza wajibu wao kwa kuwa Serikali imewaamini na kuwapa dhamana ya kusimamia rasilimali za umma kwa manufaa ya taifa.

Alieleza kuwa mapato ya Serikali bado hayaridhishi, hususan mapato yasiyo ya kodi, ambayo kwa muda mrefu hayajafanya vizuri licha ya kutegemewa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na mashirika ya umma.

Aidha, alisema wizara hiyo imepewa jukumu la kuyatambua na Mashirika  yanayoleta faida na yale yasiyoleta faida ili kuishauri Serikali hatua stahiki za kuchukua.

Aliongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Wizara itaanzisha mikataba ya utendaji kati ya ngazi mbalimbali za Serikali ili kupima ufanisi na uwajibikaji wa taasisi hizo.

Kuhusu bajeti, Dk. Akil alisema takribani shilingi bilioni 5 na milioni tano zinatarajiwa kutumika katika kuendesha shughuli za kawaida na kugharamia maeneo mengine ya kipaumbele katika mwaka wa fedha ujao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Omar Bakar, aliwataka watendaji kuanza mara moja kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kufanikisha malengo ya ziara hiyo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Zanzibar, Mhandisi Shakuru Awadh Suleiman, alisema shirika hilo linajitegemea kwa asilimia 100 huku lieleza kuwa miongoni mwa huduma wanazotoa ni intaneti kwa Serikali kwa bei ya jumla, pamoja na uuzaji wa ‘capacity’ kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar, ambapo kwa sasa wana mikonga mitatu ya intaneti.

Alisema shirika limejifunza kutoka kwa nchi nyingine zilizofanikiwa kiuchumi kwa kuwekeza katika sekta mahsusi, akieleza kuwa pamoja na Zanzibar kutegemea uchumi wa karafuu, viungo na utalii, sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa kisasa.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Bandari, Akif Ali Khamis, alisema ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani na bandari nyingine zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (ZIC), Sultan Said Suleiman, alisema shirika limejipanga kuisaidia Serikali kupitia miradi ya ujenzi wa nyumba huku akieleza kuwa tayari wamekamilisha na kuuza baadhi ya nyumba, huku wakitarajia kujenga zaidi ya nyumba 4,000 katika miradi ijayo.

Aliongeza kuwa wameandaa utaratibu wa kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kuwakodisha wafanyakazi, hatua inayolenga kuwasaidia kupanga bajeti zao na kuimarisha ustawi wao.

Naye Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar, Mhandisi Haji Mohamed Haji, alisema shirika linakabiliwa na changamoto ya miundombinu chakavu na mrundikano wa madeni, hali inayolikwamisha katika utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi wa BB mashirika ya umma na kuongeza mchango wake katika kukuza mapato ya taifa.

Scroll to Top