Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

wizara ya Fedha na Mipango

Habari & Matukio

WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Juma Malik Akil, ameridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa Kwa Fedha za Serekali.  Amesema miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali ni lazima kuzingatia mipango kazi, malipo na muda uliowekwa wa kukamilika.

Dk. Akil alisema hayo wakati akizungumza baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Mji wa Serikali Kisakasaka, AFCON City, Bandari ya Fumba na Bandari ya Mangapwani, ili kujionea hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema ufuatiliaji wa karibu wa miradi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha fedha zinazotengwa na Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na utekelezaji wake ukifanyika kwa kuzingatia viwango, mpango kazi na muda uliowekwa.

Aidha alisema  ziara hiyo imelenga  kuhakikisha fedha zinazotengwa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na matokeo yake yanaonekana kwa wananchi.

Akizungumzia mradi wa Mji wa Serikali Kisakasaka, alisema unatarajiwa kuwa na majengo ya Wizara mbalimbali za Serikali hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa nafasi za ofisi zinazozikabili taasisi za serikali.

Alisema mradi huo, ambao umeanza kutekelezwa katika kipindi cha miezi sita hadi minane iliyopita, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia takribani asilimia nane.

Kwa upande wa AFCON City ya Zanzibar, alisema mradi huo umefikia asilimia 85 ya utekelezaji, kutokana na kuanza kutekelezwa mapema ukilinganisha na baadhi ya miradi mengine.

Alibainisha kuwa  mbali na uwanja mkuu, mradi huo unahusisha viwanja vya mazoezi, eneo la kuogelea na jeti itakayowezesha vyombo mbalimbali vya usafiri wa majini kuwafikisha abiria wanaotarajiwa kufika Zanzibar kwa ajili ya michezo.

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar,  Akif Ali Khamis, alisema Bandari ya Fumba inatarajiwa kukamilisha ujenzi wa gati yake Januari 2027 na kuanza rasmi kutoa huduma Februari mwaka huo, ikiwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zenye urefu wa zaidi ya mita 350 na kina cha mita 14.5.

Alisema utekelezaji wa ujenzi wa ghati hiyo umefikia takribani asilimia 80, huku mradi mzima ukiwa umefikia asilimia 60, na awamu ya kwanza ya bandari hiyo ikitarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia takribani makontena 300,000. Alisema uwezo huo utaifanya bandari hiyo  kuwa na nafasi kubwa katika kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Malindi.

Scroll to Top