Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

wizara ya Fedha na Mipango

Uncategorized

Uncategorized

BAJETI YA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO KUWASILISWA

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil, amebainisha vipaumbele tisa vya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, vikiwemo kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kusimamia utekelezaji wa bajeti inayozingatia usawa wa kijinsia pamoja na kupitia sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma za Serikali. Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika kikao cha 30 cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Chukwani, Dkt. Juma amesema wizara hiyo itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuweka mazingira bora yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar. Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Bakari Hamad Bakar, amesema kamati hiyo inashauri wizara kuhakikisha kunakuwepo na matumizi yenye tija ya fedha za umma ili mipango iliyopangwa iweze kutekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na kukuza uchumi wa nchi. Wakati huo huo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia hotuba hiyo wamesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Akijibu hoja za wajumbe, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil, amesema Serikali itaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo yote yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Zanzibar. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliipitisha bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ya zaidi ya shilingi trilioni nane kwa ajili ya kutekelezav majukumu na vipaumbele vilivyoainishwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Uncategorized

MAKATIBU WAKUU WAKUTANA KOREA

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Ndugu Aboud Hasan Mwinyi ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha Makatibu Wakuu wa nchi za Afrika na Korea uliofanyika jijini Seoul nchini Korea. Mkutano huo umefanyika tarehe 1 na 2 Juni, 2026.

Uncategorized

MWENYEKITI WA SUKUK APONGEZA SERIKALI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Zanzibar Sukuk1 Limited, Juma Amour Mohamed, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, kwa maono na juhudi zake za kuanzisha mfumo wa hati fungani za Kiislamu (Sukuk), akisema hatua hiyo ni ya kihistoria katika kuimarisha sekta ya fedha visiwani humo.Akizungumza kuhusu mafanikio ya hatua hiyo, Juma alisema Zanzibar inalenga kuwa kitovu cha huduma za fedha za Kiislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Alieleza kuwa kuanzishwa kwa hati fungani zinazoendeshwa kwa misingi ya Sharia kumejibu kilio cha muda mrefu cha taasisi za fedha za Kiislamu zilizokuwa zikikosa fursa salama za uwekezaji. Alisema kabla ya kuanzishwa kwa Sukuk, benki na taasisi nyingine za kifedha zilizokuwa zikitoa huduma za Kiislamu zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya ukwasi mkubwa (liquidity) bila kuwa na maeneo yanayokubalika kisheria kwa uwekezaji. Hali hiyo ilisababisha kupungua kwa ufanisi wa utendaji katika soko la fedha. “Benki za Kiislamu zilikuwa na fedha nyingi lakini hazikuwa na miradi au dhamana zinazokidhi matakwa ya Sharia kwa ajili ya kuwekeza. Hii iliathiri utendaji wao na hata kuwanyima watu binafsi fursa za uwekezaji halali,” alisema. Aliongeza kuwa kuanza kwa Sukuk kumesaidia kukamilisha mnyororo wa mfumo wa fedha za Kiislamu, kwa kuwezesha taasisi na watu binafsi kuwekeza, kupata mapato halali na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Juma aliishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mpango huo, akisema umefanikiwa kama ulivyopangwa na kuleta matokeo chanya katika soko la fedha. Alibainisha kuwa mfumo wa Sukuk unatumiwa na mataifa mbalimbali duniani kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo, na si nchi za Kiislamu pekee. Alitolea mfano nchi kama United Kingdom na Belgium, ambazo pia zimetumia mfumo huo kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Sukuk1 Limited, Masoud Rashid Mohamed, alisema taasisi hiyo imeanzishwa mahsusi kusimamia miamala ya Sukuk kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, kuanzia hatua ya utoaji (issuance) hadi usimamizi wake. Alisema tayari taasisi hiyo imeanza kutoa gawio la awali kwa wawekezaji na kufanya tathmini ya utekelezaji wake ili kubaini changamoto na kuzitatua mapema. Aidha, katika bajeti ya mwaka huu, wamepanga kuanzisha mfumo wa kidijitali utakaorahisisha uendeshaji wa miamala hiyo, ambapo unatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi katika robo inayofuata ya mwaka wa fedha. Masoud alieleza kuwa taasisi mbalimbali za Serikali zimeonesha nia ya kutumia mfumo wa Sukuk kufadhili miradi yao ya maendeleo, ikiwemo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), kwa lengo la kutatua changamoto za upatikanaji wa umeme visiwani humo. Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Juma Ali Malik, ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kuhakikisha mfumo wa Sukuk unakuwa endelevu na unachangia kikamilifu maendeleo ya Zanzibar. Waziri Malik alisema kuanzishwa kwa Zanzibar Sukuk1 Limited ni hatua ya kimkakati inayolenga kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya Serikali bila kuongeza mzigo wa mikopo yenye riba. Alibainisha kuwa kupitia Sukuk, Serikali itaweza kufadhili miradi ya kimkakati ya miundombinu, nishati na huduma za jamii kwa njia inayokubalika kisheria na kidini. Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kisheria na kiudhibiti ili kuimarisha zaidi soko la fedha za Kiislamu, akisisitiza kuwa dhamira ya Zanzibar ni kujijenga kama kitovu cha huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya Sharia katika ukanda huu.

Uncategorized

Serikali Yazitaka Taasisi za Umma Ziwajibike

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil amesema mashirika ya umma yanawajibu wa kuisaidia na kuichangia Serikali kupitia gawio na mapato mengine, Dk. Akil aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea Mashirika yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa lengo la kuangalia mwenendo wa Mashirika hayo na kupokea maoni Kwa wakuu mashirika Alisema mashirika mengi hayafanyi vizuri na yameshindwa kujiendesha, hali inayopelekea  kuwa mzigo kwa Serikali, Aliwataka watendaji wa taasisi hizo kutimiza wajibu wao kwa kuwa Serikali imewaamini na kuwapa dhamana ya kusimamia rasilimali za umma kwa manufaa ya taifa. Alieleza kuwa mapato ya Serikali bado hayaridhishi, hususan mapato yasiyo ya kodi, ambayo kwa muda mrefu hayajafanya vizuri licha ya kutegemewa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na mashirika ya umma. Aidha, alisema wizara hiyo imepewa jukumu la kuyatambua na Mashirika  yanayoleta faida na yale yasiyoleta faida ili kuishauri Serikali hatua stahiki za kuchukua. Aliongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Wizara itaanzisha mikataba ya utendaji kati ya ngazi mbalimbali za Serikali ili kupima ufanisi na uwajibikaji wa taasisi hizo. Kuhusu bajeti, Dk. Akil alisema takribani shilingi bilioni 5 na milioni tano zinatarajiwa kutumika katika kuendesha shughuli za kawaida na kugharamia maeneo mengine ya kipaumbele katika mwaka wa fedha ujao. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Omar Bakar, aliwataka watendaji kuanza mara moja kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kufanikisha malengo ya ziara hiyo. Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Zanzibar, Mhandisi Shakuru Awadh Suleiman, alisema shirika hilo linajitegemea kwa asilimia 100 huku lieleza kuwa miongoni mwa huduma wanazotoa ni intaneti kwa Serikali kwa bei ya jumla, pamoja na uuzaji wa ‘capacity’ kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar, ambapo kwa sasa wana mikonga mitatu ya intaneti. Alisema shirika limejifunza kutoka kwa nchi nyingine zilizofanikiwa kiuchumi kwa kuwekeza katika sekta mahsusi, akieleza kuwa pamoja na Zanzibar kutegemea uchumi wa karafuu, viungo na utalii, sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa kisasa. Naye Mkurugenzi wa Shirika la Bandari, Akif Ali Khamis, alisema ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani na bandari nyingine zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba. Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (ZIC), Sultan Said Suleiman, alisema shirika limejipanga kuisaidia Serikali kupitia miradi ya ujenzi wa nyumba huku akieleza kuwa tayari wamekamilisha na kuuza baadhi ya nyumba, huku wakitarajia kujenga zaidi ya nyumba 4,000 katika miradi ijayo. Aliongeza kuwa wameandaa utaratibu wa kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kuwakodisha wafanyakazi, hatua inayolenga kuwasaidia kupanga bajeti zao na kuimarisha ustawi wao. Naye Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar, Mhandisi Haji Mohamed Haji, alisema shirika linakabiliwa na changamoto ya miundombinu chakavu na mrundikano wa madeni, hali inayolikwamisha katika utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo. Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi wa BB mashirika ya umma na kuongeza mchango wake katika kukuza mapato ya taifa.

Scroll to Top