NYENZO YA BAJETI YAZINDULIWA
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema kwa kutambua umuhimu wa jinsia na wazee katika maendeleo ya kijamii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 imetenga bilioni 449 katika kutekeleza mpango huo. Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Juma Malik Akil aliyasema hayo wakati akizindua nyenzo za bajeti inayozingatia jinsia (GRV) katika ukumbi wa Wazee Sebleni. Alisema hicho ni kiwango kikubwa ambacho kitawezesha kutekeleza jambo hilo kwa ufanisi kwani bajeti ya mwaka 2025/2026 ilitenga shilingi bilioni 70 pekee. Alifahamisha kuwa uzinduzi huo una umuhimu wa kipekee kwani unafanyika wakati Zanzibar inahitimisha utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum) wa miaka mitano, 2021–2026. “Uzinduzi huu ni miongoni mwa mafanikio muhimu ya utekelezaji wa ahadi hizo na unaonesha dhamira ya serikali ya kuimarisha usawa wa kijinsia na uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma,” alisema. Alisema bajeti ndio nyenzo kuu ya serikali katika kutekeleza sera na mipango ya maendeleo kwani kupitia bajeti, serikali huamua namna rasilimali zitakavyogawiwa na huduma zitakavyotolewa kwa wananchi. Aidha alisema ni muhimu kuhakikisha kuwa maamuzi hayo yanazingatia mahitaji halisi ya wanawake, wanaume, wavulana na wasichana ili kuwa na maendeleo jumuishi na yenye manufaa kwa wote. Dk. Malik alisema nyenzo hizo zitachangia utekelezaji wa Dira ya Zanzibar 2050, Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP), Sera ya Jinsia ya Zanzibar ya mwaka 20216 na Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto awamu ya pili wa mwaka 2025/2026– 2030. Waziri Malik alisisitiza kuwa uzinduzi wa vifaa hivyo si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya utekelezaji hivyo alizihimiza wizara, Idara na taasisi za serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Baraza la Wawakilishi, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinatumika kikamilifu katika majukumu yao ya kila siku Alisema sasa kuna wizara tisa ambazo zinatekeleza mpango huo kwa majaribio na anaamini zitaweza kuongezeka ili kufikia katika kutekelekeza ngazi yote ya kitaifa. Aliipongeza UN Women kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa serikali katika kuimarisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na kuendeleza utawala bora na maendeleo jumuishi, Umoja wa Ulaya (European Union) na Gates Foundation kwa msaada wao wa kifedha uliowezesha maandalizi, mapitio na ukamilishaji wa vifaa hivyo muhimu. Naye, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Anna Attanas Poul, alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu kwani itaimarisha uwezo wa wizara na wadau wake kuhakikisha kuwa masuala ya kijinsia yanazingatiwa kikamilifu katika mipango, bajeti na utekelezaji wa programu za maendeleo. Alisema alisema UN Women kwa kushirikiana na washirika wake wameendelea kuiunga mkono serikali katika kuimarisha Bajeti Inayozingatia Jinsia na usimamizi wa fedha za umma unaozingatia usawa na ujumuishi. Kwa upande wake Mwakilishi wa UN Women Tanzania, Catharine Gifford, alisema bajeti inayozingatia jinsia ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinawanufaisha wananchi wote kwa usawa bila kujali jinsia. Aliipongeza SMZ kwa juhudi zake za kuingiza masuala ya kijinsia katika mifumo ya mipango na bajeti kwani bajeti inayozingatia jinsia sio bajeti maalumu kwa wanawake au wanaume pekee bali ni mfumo unaolenga kuhakikisha sera, mipango na matumizi ya fedha za umma yanazingatia mahitaji ya wanawake, wanaume, wasichana na wavulana kwa usawa. Alibainisha kuwa mbinu hiyo husaidia kubaini makundi yanayonufaika na matumizi ya umma na yale yanayoweza kubaki nyuma katika mchakato wa maendeleo. Hivyo, aliahidi kuwa UN Women itaendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha masuala ya kijinsia yanaingizwa kikamilifu katika upangaji wa mipango, ugawaji wa bajeti na utoaji wa huduma kwa wananchi wote.









