Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akil amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Mashirikiano ya Kimataifa la Korea (KOICA) Mkurugenzi Manshik Shin na Ujumbe wake katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais- Fedha na Mipango Mazungumzo hayo yamelenga katika kuimarisha mashirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Korea Kusini kupitia Shirika Hilo. Kikao hicho kilihudhuriwa na Sekta mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwemo Sekta ya Utalii, Elimu, Uchumi wa Buluu, Kilimo, Uwekezaji na Biashara.
Dkt. Juma Malik amemuhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa Zanzibar ipo tayari kushirikiana na Korea katika kuimarisha mashirikiano yaliyopo ili kuweza kutatua changamoto.
Dkt. Juma amemesema kuwa Zanzibar imewasilisha maandiko ya Miradi 15 kwa mazingatio ya kupatiwa ufadhili kutoka katika Shirika hilo la KOICA na miradi hiyo ina lengo la kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP) ili kuweza kuleta maendeleo kwa Wananchi wa Zanzibar.
Nae, Mkurugenzi Manshik Shin aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano ambayo imekuwa ikiipatia Korea katika kuimarisha mahusiano baina ya Korea na Zanzibar. Mkurugenzi huyo aliahidi kufanyia kazi maeneo ambayo yamewasilishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuyapatia ufadhili na ameahidi kushirikiana na Sekta mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha mashirikiano ili kuleta maendeleo na mafanikio Nchini.
Mkurugenzi Manshik ameahidi kuyafanyia kazi maombi yaliyowasilishwa katika kikao hicho ikiwemo kuisaidia Zanzibar katika kuipatia ufadhili wa Elimu ya Juu kwa wafanyakazi wa Serikali ikiwemo Shahada ya Uzamili na Uzamivu, Kuimarisha mashirikiano ya Kisekta, Kuichangia mfuko wa Ufadhili wa Sekta ya Afya Pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango alisositiza kwa kuliomba Shirika hilo kuendelea kuisaidia Zanzibar na kuzingatia maombi ambayo yamewasilishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sekta mbalimbali na kuahidi kuwa milango ya Zanzibar ipo wazi wakati wote kuhakikisha inaimarisha mashirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Ofisi ya Rais- Fedha na Mipango